DW-World
Iraq imekanusha na kuyataja kuwa uongo mtupu, madai ya Marekani na Uingereza kuwa ina silaha za maangamizi, na kwamba ina uwezo wa kuunda silaha za kinuklia.
Gazeti la chama cha Baath kinachotawala Iraq, linalojulikana kama Ath-Thawra, limesema kuwa ahadi zote zilizofanywa na rais George W. Bush wa Marekani, na waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair, kwamba watatoa ushahidi kuonyesha kuwa Iraq ina silaha za maangamizi, ni uongo mtupu.
Rais Bush pamoja na Waziri mkuu Blair, walikutana camp David, mwishoni mwa juma lililopita, katika mazungumzo ya kutafuta kuungwa mkono na mataifa ya ulimwengu, juu ya swala la marekani kuishambulia Iraq kijeshi, ili kumuondoa mamlakani rais Saddam Hussein. Leo taasisi ya masomo ya mikakati ya silaha - International Institute of Strategic Studies, imesema kuwa uundaji wa silaha za kinuklia, za kemikali, na biologia ndilo limekuwa kengo kuu katika serikali ya Baghdad.
Akitoa taarifa ya taasisi hiyo iliyoko London, mkurugenzi wake John Chipman, alisema kuwa jumuia ya kimataifa ina jukumu la kukabiliana na utawala huo wa Iraq pamoja na silaha zake.
Chipman aliwaambia waandishi wa habari kuwa vikwazo vya kivita na ukaguzi vimerudisha nyuma uundaji wa silaha za maangamizi nchini Iraq, lakini havikuokomesha.
Hata hivyo gazeti rasmi nchini Iraq, Al-Jamhuriya limesema kuwa Bush na Blair, hawana habari zozote wanazoweza kutoa hadharani, kuhusu silaha nchini Iraq. Makamu wa rais wa Iraq Taha Yassin Ramadan, amesema kuwa iwapo Marekani itadhubutu kuishambulia Iraq, basi itapata pigo na aibu kubwa. Akinukliwa na magazeti rasmi, Ramadan aliwaambia waandishi wa habari wa kituruki waliomtembelea kuwa, watu wa Iraq wataungana pamoja dhidi ya shambulizi lolote la kigaidi kutoka Marekani, na kuhakikisha kuwa Marekani imeaibika. "Chuki dhidi ya Marekani inaendelea kuongezeka kote ulimwenguni, kutokana na tabia yake ya kuyaingilia masuala ya nchi zingine." Akasema. Aliendelea kusema kuwa mwanadiplomasia mmoja wa Iraq aliye Jordan, anatazamiwa kuwa na mazungumzo na mfalme Abdullah wa pili.
Mazungumzo hayo ni baadhi ya juhudi za Iraq za kutafuta kuungwa mkono dhidi ya mashambulizi ya Marekani.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari kutoka Uturuki, Ramadan pia aliionya Uturuki dhidi ya kupeleka majeshi yake katika eneo la wakurdi, kusini mwa Iraq. Akasema kuwa Iraq inapinga kuwepo kwa majeshi yoyote ya kigeni katika ardhi yake.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, mkuu wa majeshi ya Uturuki, Generali Hilmi Ozkok, alinukuliwa na shirika moja la habari nchini Uturuki, akikiri kuwa kulikuwa na majeshi ya kituruki katika eneo la wakurdi, kaskazini mwa Iraq. Hata hivyo alikataa kutoa maelezo zaidi kuhusu majeshi hayo.
Kuhusu swala la marekani kuishambulia Iraq kijeshi, kiongozi wa Palestina, Yasser Arafat, ametoa mwito kuwepo na suluhisho la kisiasa la kimataifa, kwa mzozo wa Iraq, hasa wakati huu ambapo Marekani inazidisha vitisho vyake dhidi ya utawala wa Saddam Hussein. Suluhisho kama hilo, akasema, ni wajibu wa ulimwengu mzima na litasaidia kupatikana kwa amani katika eneo hilo pamoja na mashariki ya kati.